Maisha na muziki
Mbaraka Mwinshehe Mwaruka alizaliwa mjini Morogoro akiwa mtoto wa pili kati ya watoto 12. Baba yake Mwinshehe Mwaruka alikuwa Mluguru msomi na karani katika mashamba ya katani, na mama yake alikuwa Mngoni. Kati ya hao kumi na mbili, ni yeye na wadogo zake Zanda na Matata ndio walikuwa wanamuziki, Zanda alikuwa mwimbaji, akiimba pia nyimbo za Kizungu katika bendi ya Morogoro na Matata alikuwa mpiga drum pia bendi hiyohiyo. Kutokana maelezo ya familia, babu yake Mbaraka alikuwa wa kabila la Wadoe wa Bagamoyo na alipelekwa Mzenga (Kisarawe) akawe chifu wa huko na wakoloni. Huko akaoa wake tisa na kupata watoto zaidi ya hamsini akiwemo baba yake Mbaraka. Mbaraka alisoma mpaka kidato cha tatu na kuacha shule ili awe mwanamuziki.